Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Baraza Kuu la Kiislamu la Alawi nchini Syria na nje ya nchi, kwa kutoa tamko, limelaani vikali jinai za kigaidi zinazoendelea kufanywa dhidi ya raia wa dhehebu la Alawi, na kuzitaka mamlaka tawala za juu ziwajibike kikamilifu na wa moja kwa moja kutokana na vitendo hivi, na kusisitiza kuwa; kinachoendelea ni matokeo yasiyoepukika yanayotokana na sera za ubaguzi, uchochezi na matumizi ya vurugu.
Katika tamko hilo, Baraza hilo limeelezea kushambuliwa kigaidi Msikiti wa Imamu Ali bin Abi Talib (amani iwe juu yake) uliopo katika eneo la Wadi al-Dhahab katika mji wa Homs, ambapo hadi sasa zaidi ya watu 30 wamejeruhiwa vibaya, wakiwemo mashahidi 12 miongoni mwao ni watoto, wanaume na wazee.
Baraza Kuu la Alawi limeutazama uvamizi huo kama muendelezo wa ugaidi wa kitakfiri uliopangwa dhidi ya dhehebu la Alawi na madhehebu mengine ya Syria, kwa namna inayozidi kuongezeka.
Baraza hilo limebainisha kuwa; asili ya shambulio hili inafanana kikamilifu na matukio ya awali ya kigaidi, ikiwemo mlipuko uliolenga wanajeshi wa Marekani katika eneo la al-Tanf, uliofanywa na mshambuliaji wa kujitoa mhanga anayehusishwa na mamlaka tawala, na kusababisha vifo vya askari watatu; pamoja na mlipuko wa Kanisa la Mar Elias katika mtaa wa al-Duwaila mjini Damascus. Hili linathibitisha kuwa mhusika ni mmoja, na linakanusha madai yoyote ya kwamba; uhalifu huu ni matukio ya mtu mmoja mmoja au makosa yaliyojitenga.
Baraza Kuu la Alawi limeitaka jumuiya ya kimataifa, Baraza la Usalama, mashirika ya kimataifa na watoa maamuzi duniani kuchukua hatua za haraka na za maamuzi ili kusitisha umwagaji huu wa damu, na kuliweka eneo la pwani ya Syria chini ya ulinzi wa kimataifa.
Baraza hilo, huku likionya kwamba vitendo hivi vya kihalifu havitapuuzwa kwa muda mrefu, na kwamba kuendelea kwake kutakabiliwa na jibu linalolingana na ukubwa wa dhulma na uchokozi uliofanywa, limesisitiza kuwa subira juu ya damu na heshima ya mataifa ina mipaka ambayo hairuhusiwi kuvukwa.
Maoni yako